Mgeni rasmi katika hafla fupi ya kuwatunuku vyeti pamoja na kufunga mafunzo ya michezo ya riadha kwa watoto ' Kids athletics' Ndg. Fidelis Kyarwenda akizungumza na walimu walioshiriki mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwenye uwanja mkuu wa michezo uliopo katika mji mdogo wa Kibaya, wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara.
Afisa michezo ( W) bibi Juliana Mtei akizungumza wakati wa hafla hiyo.
..........HABARI KAMILI...........
Mgeni rasmi katika hafla fupi ya kuwatunuku vyeti pamoja na kufunga mafunzo ya michezo ya riadha kwa watoto ' Kids athletics' ambaye pia ni Mdhibiti mkuu wa ubora wa shule wilaya ya Kiteto ndugu Fidelis Kyarwenda amewataka walimu kutouweka mifukoni ujuzi walioupata kupitia mafunzo hayo,badala yake waende wakawafundishe wanafunzi wao.Kyarwenda ameyasema hayo Jumatatu ya tarehe 05/11/2018 katika uwanja mkuu wa michezo uliopo ndani ya mji mdogo wa Kibaya, wilaya ya Kiteto, Mkoani wa Manyara.
Akizungumza wakati wa hotuba yake Kyarwenda amesema “ mmeahidi wenyewe hapa kwamba mafunzo mliyoyapata hamtayaweka mifukoni,bali mtakwenda kuwafundisha wanafunzi wenu.Mkifanya hivyo hamtakuwa mmeiweka rehani michezo, watoto wetu watacheza. Msiende kutafuta sababu ya kuhalalisha kutowafundisha watoto, mkafundishe watoto na kuwasimamia kama mlivyofundishwa na kusimamiwa hadi mkaelewa”.
Kyarwenda ameendelea kusema kwamba michezo ambayo walimu hao wamejifunza, wakienda kuifundisha katika shule zao, na watoto wakaelewa ,wataipenda , ari ya kupenda shule itaongezeka, itakuwa chachu ya kupunguza utoro shuleni, kwa sababu hata watoto wasiopenda kwenda shule, wasiofanya vizuri darasani ,michezo itawavuta kwenda shule .
Kyarwenda amesema kwamba kazi yake ni kusimamia ubora wa elimu, na kwa sababu michezo mashuleni ni sehemu ya elimu, atasimamia kikamilifu kuhakikisha kwamba michezo hiyo inafundishwa katika shule zote ambazo zimeleta walimu kwenye mafunzo hayo. Aidha amemuomba Afisa michezo wa wilaya kumpatia orodha ya washiriki wote wa mafunzo, ili atakapokuwa anakwenda kufanya ukaguzi ,afuatilie kama wanafunzi wanafundishwa michezo hiyo.
Kadhalika Kyarwenda amewataka walimu hao kujenga mahusiano mazuri mahali popote pale watakapokuwa.Amesema kwamba wamejifunza michezo uwanjani, lakini pia wamejifunza mambo mengi, wameona jinsi mkufunzi wao alivyo na mahusiano mazuri na watu, hadi kufikia hatua ya kuwatafutia nafasi za chuo kwa wale watakaokuwa tayari kujiendeleza katika fani ya michezo,na wao wanapaswa kuwa na mahusiano mazuri, ili pale wanapokuwa wanahitaji kufanya jambo fulani waweze kulifanya kwa urahisi.
Kyarwenda pia amewasifu walimu hao kwa nidhamu waliyoionyesha wakati wote wa mafunzo. Amewaambia kwamba walitumwa kujifunza michezo ili wakafundishe wanafunzi, wamefanya mafunzo vizuri, wamekuwa na nidhamu wakaweza kujifunza, hivyo kwa uwiano huohuo, nidhamu hiyohiyo ambayo wameionyesha wakati wa mafunzo, wakaionyeshe katika kuwafundisha wanafunzi wao ili matunda ya mafunzo hayo yaonekane kwenye shule zao.
Kyarwenda pia amezungumzia suala la vifaa vya michezo, amesema kwamba vifaa vyote ambavyo vimetumika katika mafunzo hayo ni vya kisasa, vifaa ambavyo katika mazingira wanakotoka walimu hao havipo, lakini wao kama walimu wanatakiwa kufaragua zana za kufundishia, wakafarague vifaa vya kufundishia michezo hiyo, watoto wasiache kucheza kwa sababu vifaa hivyo havipo.
Sambamba na kuwataka walimu hao kufaragua vifaa vya kufundishia michezo hiyo, Kyarwenda amesema kwamba suala la kuwa na vifaa vya michezo ni la muhimu, hivyo atashirikiana na Afisa michezo wa wilaya kulipeleka suala hilo kwa Mkurugenzi ili kwa pamoja waone ni kwa namna gani vifaa hivyo vinaweza kupatikana .
Naye afisa michezo wa wilaya ya Kiteto mama Juliana Mtei,ameahidi kuyasimamia na kufuatilia yote ambayo wamekubaliana katika mafunzo hayo.Huku akisisitiza kwamba walimu wote ambao wameshiriki katika mafunzo hayo,watapewa kipaumbele wakati wote ambapo mafunzo na shughuli mbalimbali za michezo zitakuwa zikifanyika,iwe ndani ya wilaya au za kwenda nje ya wilaya.
Katika hatua nyingine walimu walioshiriki mafunzo hayo wameshukuru kwa kupata fursa ya kushiriki, pia wamemshukuru mkufunzi kwa kazi nzuri aliyoifanya, kazi ambayo imewawezesha kufahamu michezo mingi,ambayo kabla ya mafunzo hayo hawakuwa wakiifahamu.Aidha wamemuomba asiache kufika Kiteto kutoa mafunzo ,kila wakati anapopata nafasi,kwani wanaamini kwamba bado anayo mengi ya kuwafundisha, ili waweze kuwa walimu bora wa michezo kwa siku za usoni.
Kwa mara ya kwanza walimu kutoka shule za msingi na sekondari wilayani hapa wameweza kukusanyika pamoja na kupata mafunzo mbalimbali ya michezo ya watoto.Jumla ya walimu 91 wameshiriki mafunzo hayo ya siku tatu na kutunukiwa vyeti .
.......MWISHO..........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa