Mbunge wa Kiteto Mhe. Emmanuel Papian akizungumza na wakazi wa kijiji cha Kimana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Kimana mwishoni mwa wiki.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimana akifungua Mkutano wa Mbunge wa Kiteto Mhe. Emanuel Papian kuzungumza na wananchi katika kijiji cha Kimana.
Wakazi wa kijiji cha Kimana ,kata ya Partimbo, wilaya ya Kiteto wakiwa wamekusanyika kumsikiliza Mbunge wao Mhe. Emmanuel Papian katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Wakazi wa kijiji cha Kimana wakiwasilisha kero zao kwa Mbunge wa Kiteto Mhe. Emmanuel Papian katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
.....HABARI KAMILI........
Mbunge wa Kiteto Mheshimiwa Emmanuel Papian amewataka wakazi wa Kiteto kudumisha amani kwa kuheshimu mipango ya matumizi bora ya ardhi waliyojipangia katika vijiji vyao . Mhe. Papian ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara kijijini Kimana mwishoni mwa wiki.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini Kimana, Mheshimwa Papian amesema “ Kwa sasa hatutarajii kusikia migogoro ya wakulima na wafugaji, maana wakulima wako sehemu yao, na wafugaji wako sehemu yao.Ninachotarajia kusikia ni mkulima amevuna, mabua amempa mfugaji .Ikitokea kwa bahati mbaya ng’ombe zimeingia kwenye shamba la mkulima,mkulima na mfugaji wakae ,wazungumze walipane ,familia ziishi kwa usalama na amani”.
Mheshimiwa Papian amesema kwamba japokuwa utaratibu ulishawekwa kuhusu suala ya kuchunga mifugo kwenye mashamba,kwamba mtu atakayechunga kwenye shamba tathmini ya uharibifu ifanyike,mfugaji alipe fidia ya uharibifu , wenyeviti wa vijiji waorodheshe majina ya wafugaji wanaochungia kwenye mashamba ili kuweza kupata majina hayo na kufahamu ni wakina nani wanaochochea uvunjifu wa amani ili waweze kushughulikiwa. Akisisitiza kuhusu hilo Mhe. Papian amesema ‘’ Mwenyekiti wa kijiji anatakiwa atafute daftari,mkulima ukilishiwa shamba lete jina la aliyechungia shamba kwa mwenyekiti,ukiwa na shahidi wako,mwenyekiti ataandika jina hilo kwenye daftari, na wewe uliyelishiwa pamoja na shahidi wako mtasaini. Mkuu wa mkoa anataka kupata orodha ya watu wanaochunga mifugo katika mashamba ya watu”.
Katika hatua nyingine wakazi wa kijiji cha Kimana wameeleza kuhusu suala la nyumba za walimu zilizopo katika shule ya msingi Kimana kugeuka mahame baada ya walimu wa shule hiyo waliokuwa wakiishi katika nyumba hizo kuhama na kuziacha nyumba hizo zikiwa hazina mtu wa kukaa. Akijibu kuhusu kero hiyo Mhe Papian amemtaka mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo kufuatilia suala hilo kuhakikisha kwamba walimu wanaishi katika nyumba za shule ili kuinua hali ya taaluma shuleni hapo.
Katika mkutano huo wanakijiji wamewasilisha kero mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji, uchache wa vyumba vya madarasa, ukosefu wa zahanati , na suala la barabara, ambapo kwa upande wa suala la zahanati, Mhe. Papian amewataka wananchi wa kijiji hicho kutofikiria kujenga zahanati,badala yake wafikirie na kuweka malengo ya kujenga kituo cha afya kwa sababu uwezo wa kujenga kituo cha afya wanao.Na kwamba wafanye utaratibu wa kuandaa harambee ambapo wakulima na wafugaji wote katika eneo hilo watashiriki katika harambee hiyo kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha afya, na yeye mwenyewe ataalika wabunge wenzake kushiriki katika harambee hiyo ili fedha zipatikane, ujenzi uanze mara moja.
Katika kuhakikisha kwamba jambo hilo linatekelezeka ameutaka uongozi wa kijiji hicho kutenga eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Kwa upande wa barabara wanakijiji hao wamesema kwamba barabara iliyokuwa ikitumika zamani ambayo kwa sasa haitumiki tena , ndiyo iliyokuwa fupi na rahisi kwao kutoka na kuingia kijijini hapo, tofauti na barabara inayotumika sasa ambayo ni ndefu sana,jambo linalowasababishia usumbufu mkubwa hususani wanapokuwa na wagonjwa, kwani hulazimika kulipa gharama kubwa sana za usafiri, tofauti na wakati walipokuwa wakitumia barabara ya zamani.Mhe. Papiani ametoa majibu ya maswali yote,ambapo ameahidi kushughulikia kero zote zilizowasilishwa na wanakijiji hao ili waweze kuishi vizuri.
Mhe. Papian yuko katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi katika vijiji mbalimbali jimboni mwake. Ziara hiyo inafanyika kwa muda wa siku saba,ambapo katika siku ya kwanza ya ziara yake hiyo, miongoni mwa vijiji alivyovitembelea ni kijiji cha Kimana.
................ MWISHO.................
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa