Mkuu wa Wilaya ys Kiteto, SSI. Mbaraka Batenga, amewaasa wananchi wa Kiteto kuuenzi na kuuthamini Uhuru wa nchi ili kuliendeleza Taifa.
Hayo ameyasema Desemba 9,2023 katika Ukumbi wa Maktaba ya Wilaya kwenye maadhimisho ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo katika Wilaya ya Kiteto yaliadhimishwa kupitia mdahalo maalumu wa kujadili mafanikio ya nchi katika miaka 62 ya Uhuru.
Mh. Batenga alisema kwamba kwavile uhuru upo, watu wanaweza wasione umuhimu wake ila pale ambapo uhuru umetoweka ndipo utajulikana umuhimu wa uhuru.
“Lazima tuulinde uhuru wetu maana hakuna mtu atakupa uhuru halafu asikunyemelee, tuulinde uhuru ili hata yule aliyetupatia aone kua tulikua na dhamira nzuri ya kuudai uhuru ili kuliendeleza Taifa letu”, aliongeza Mh. Batenga.
Mdahalo huo ambao uliudhuriwa na watumishi, viongozi wa taasisi mbalimbali,wanafunzi na wananchi mbalimbali wakiwemo wazee maarufu wilayani hapo; ulitanguliwa na majaribio mbalimbali ya kikemia, fizikia na bailojia ambayo yalioneshwa na wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Kiteto.
Akiongea katika mdahalo huo, Mkurugenzi Mtendaji (W) Kiteto CPA. Hawa Abdul Hassan, amesema kwamba moja ya mafanikio katika miaka 62 ya Uhuru ni pamoja na kuboreshwa kwa sekta ya elimu kupitia vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
“Kabla ya kuanza mjadala huu wanafunzi wametuonesha majaribio ya kisayansi kwa vitendo. Ila miaka ya nyuma majaribio hayo yalifanywa kwa nadharia tu” aliongeza Mkurugenzi Mtendaji huyo.
Nae mmoja ya wazee wa wilaya hiyo Mzee Lembulung Ole Kosiando alisema kwamba uhuru unatakiwa kuambatana na umoja na amani ila bila vitu hivyo viwili uhuru unakua hauna maana.
Vilevile Mzee maarufu wilayani hapo Mzee Mbaruku Said Muya alieleza jinsi ambavyo nchi imepiga hatua katika eneo la utawala na kueleza jinsi utawala wa serikali enzi za mkoloni ambao ulikua unaongozwa na mkuu wa wilaya ambapo mkuu wa wilaya alibeba majukumu yote na alitawala pia kimabavu.
“Enzi hizo mkuu wa wilaya ndio alikua kila kitu, yeye ndo hakimu, yeye daktari na ulikua unaweza kwenda ofisini kwake unashida ya kuonana nae ila ukaambiwa ana kazi nyingi na hapo huenda katulia tu anasoma gazeti hivyo itakupasa umsubiri mpaka amalize kusoma gazeni lake ndipo umuone kueleza shida yako” alisema Mzee Muya.
Kauli Mbiu ya Miaka 62 ya Uhuru ni “UMOJA NA MSHIKAMANO NI CHACHU YA MAENDELEO YA TAIFA LETU”.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa