Wananchi wa kijiji cha Ngabolo wilayani Kiteto, wameaswa kuwapa ushirikiano madaktari na wahudumu wa afya wote wanawapa huduma katika zahanati ya Ngabolo.
Rai hiyo imetolewa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndg. Ismail Ali Ussi, Julai 13, 2025 wakati wa uzinduzi jengo jipya la zahanati hiyo.
Akiongea baada ya kukagua zahanati hiyo, kiongozi huyo amesema kwamba amefurahishwa kujionea huduma ambazo zinatotelewa katika zahanati hiyo ikiwemo huduma ya kujifungua na huduma ya mama na mtoto.
Aidha kiongozi huyo aliipongeza halmashauri kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa jengo hilo jipya kwani hiyo ni dhamiria ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za afya.
"Tunaposema Mwenge wa Uhuru unaleta upendo mahali ambapo hakuna upendo, matumaini ambapo hakuna matumaini basi tunamaanisha maana zahanati hii inaleta hayo", aliongeza Ndg. Ussi.
Mbali na hayo kiongozi huyo alisema kwamba serikali imetumia fedha nyingi ili wananchi wasiweze kusumbuka hivyo alitoa rai kwa wananchi hao kulinda na kutunza miundombinu yote katika jengo hilo jipya na kuwapa ushirikiano madaktari na wahudumu wote wa afya kwenye zahanati hiyo kwani wanafanya kazi kubwa.
Jengo hilo jipya la zahanati ya Ngabolo ambalo linalenga kutoa huduma kwa wananchi 5225, limezinduliwa na Mwenge wa Uhuru na ujenzi wa jengo hilo umegharimu kiasi cha fedha milioni 126.
Kukamilika na kuzinduliwa kwa mradi huo kutasaidia kupatikana kwa huduma bora katika miundombinu iliyo bora na yenye kukidhi mahitaji ya sasa na hivyo kupunguza au kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na uzazi, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.
Aidha mradi huu pia utasaidia kutoa huduma za lishe, mapambano dhidi ya UKIMWI, malaria na afua zingine za afya kwa wanachi katika mazingira mazuri pamoja na watoa huduma wa zanahati hiyo.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa