Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Emmanuel Mwagala ( aliyesimama) akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.Maadhimisho hayo kiwilaya yamefanyika katika kijiji cha Ngipa ,kata ya Engusero.
Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya,kaimu Mkurugenzi Mtendaji pamoja na wananchi kutoka maeneo na taasisi mbalimbali wilayani Kiteto wakipanda miti kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
Afisa tarafa ya Kibaya Bi. Dhulfa Laizer akiwasilisha hotuba ya Mkuu wa wilaya ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.
Diwani wa kata ya Engusero Mhe. Solomoni Mbulunyuku akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.
Mmoja kati ya wajumbe wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Kiteto ambaye pia ni diwani V/M Tarafa ya Kibaya Mhe. Ngaisi akizungumzia mimba za utotoni wakati wa maadhimisho hayo.
Dkt. Mwanaidi Shabani kutoka hospitali ya wilaya ya Kiteto akizungumza kuhusu uzazi salama wakati wa maadhimisho hayo.
Wanawake kutoka maeneo mbalimbali wilayani Kiteto wakiwa wamekusanyika katika maadhimisho hayo.
Wanawake wakicheza muziki wakati wa maadhimisho hayo.
Vikundi vya wanawake vya ngoma za asili vikitumbuiza katika maadhimisho hayo.
................ HABARI KAMILI..........
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Emmanuel Mwagala amewataka wanawake wilayani Kiteto kutambua na kukaa kwenye nafasi yao sawasawa. Mwagala ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika kijiji cha Ngipa kata ya Engusero .
Akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi Mwagala amesema “ Mtoto akizaliwa mwalimu wake wa kwanza ni mama,ninyi wanawake mna nafasi kubwa na umuhimu mkubwa sana katika maisha ya mwanadamu hapa duniani,lakini bado wengi wenu hamjatambua umuhimu wenu na kuchukua nafasi yenu na kuifanyia kazi.Tambueni nafasi yenu muitendee haki.Ulimwengu ulishatambua umuhimu wenu katika jamii tangu zamani.Na ndio sababu muafrika wa kwanza msomi aliyeitwa daktari Agrey alifika mahali akasema kwamba ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii”
Mwagala amewataka wanawake kuachana na dhana zinazolenga kumdhoofisha mwanamke na kumdhalilisha mwanamke .Hapa anasema “ Achaneni na nadharia ambayo ililetwa na watu wachache ambao walimtazama mwanamke kama chombo cha starehe, kiumbe dhaifu ambaye kila anachokifanya ni kwaajili ya kumpendeza na kumfurahisha mwanaume.Ondokeni huko, achaneni na hiyo dhana potofu , mna nguvu kubwa ambayo mkiamua kwa dhati kukaa kwenye nafasi yenu na mkaituia vizuri hiyo nguvu iliyomo ndani yenu mtaweza kufanya mambo makubwa sana”.
Kadhalika Mwagala amewataka wanawake kusimama kidete kuhakikisha kwamba watoto wakike wanakwenda shule kama ilivyo kwa watoto wakiume.Mwagala amesema kwamba kwa miaka mingi mtoto wa kike amekuwa akitazamwa kama mtu wa kufanya kazi za nyumbani, na kitega uchumi cha wazazi,hali hiyo ya kumtazama kama kitega uchumi imesababisha watoto wa kike kuozeshwa wakiwa na umri mdogo ili wazazi wapate mahari, bila kujali kwamba kufanya hivyo kunawanyima watoto wa kike haki ya kusoma, na kunakatisha malengo yao na hatimae kuharibu kabisa mustakabali wa maisha yao.
Naye Kaimu Afisa maendeleo ya jamii wilaya ndugu Steven Mafuru amesema kwamba siku ya wanawake duniani imewekwa kwa lengo la kuikumbusha jamii kutambua thamani na nafasi ya mwanamke katika jamii.Hivyo katika kuadhimisha siku hiyo ni vema jamii ikaendelea kuelimishwa na kukumbushwa nafasi ya mwanamke katika jamii , mwanamke akipewa nafasi na fursa ana uwezo wa kufanya mambo makubwa.Atambuliwe, athaminiwe na aheshimiwe.
Katika hatua nyingine Umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi wilayani hapa wamewataka wanawake kutofumbia macho tabia na mienendo ambayo inachochea mimba za utotoni,badala yake wasimame kwa nguvu moja kukemea vitendo hivyo ili kutokomeza tatizo la mimba za utotoni ,tatizo ambalo katika miaka ya hivi karibuni limeendendelea kushika kasi.
Aidha Daktari Mwanaidi Shabani kutoka hospitali ya wilaya ya Kiteto amewataka wanawake kujitendea haki wakati wanapokuwa wajawazito kwa kuanza kliniki mara tu wanapohisi kwamba ni wajawazito, na wakati wa kujifungua unapofika waende kujifungulia katika vituo vya afya au hospitali,wasijifungulie majumbani kwa sababu wakati wa kujifungua hatari ni nyingi sana, hivyo wanapojifungulia majumbani wanahatarisha maisha yao na ya watoto wao.
Katika maadhimisho hayo wanawake wa kijiji cha Ngipa wamewasilisha kero zao kwa mgeni rasmi ambapo kero hizo ni kukosa huduma ya maji katika maeneo ya karibu, hali ambayo inawalazimu kutembea umbali mrefu kutafuta maji.Ukosefu wa zahanati katika kijiji chao,hivyo kulazimika kufuata huduma za matibabu katika makao makuu ya kata (Engusero)katika hili wamemuomba mgeni rasmi awasaidie jengo lao la zahanati ambalo limeshapauliwa limaliziwe li huduma za afya ziweze kupatikana kijijini hapo.Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo bibi Dhulfa Laizer ameahidi kuzifikisha kero hizo kwa mkuu wa wilya ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Tarehe 8 Machi kila mwaka ni siku ya wanawake duniani, ambapo nchi zote wanachama wa umoja wa mataifa huadhimisha siku hiyo.Mwaka huu 2019 wilayani Kiteto, maadhimisho hayo hayo yaliambatana na zoezi la upandaji miti .
...........MWISHO............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa