Makamu mwenyekiti wa Jukwaa la wanawake Kiuchumi na Mtoa msaada wa sheria kutoka Taasisi ya Msaada wa Sheria ( WILAC) Bibi Mwadawa Ally akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.Maadhimisho hayo kiwilaya yamefanyika katika kijiji cha Ngipa - kata ya Engusero.
Wananchi kutoka katika maeneo na taasisi mbalimbali wakiwa katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.
.................HABARI KAMILI........
Makamu mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Kiuchumi wilaya ya Kiteto na mtoa msaada wa sheria kutoka katika Taasisi ya Msaada wa Sheria (WILAC) bibi Mwadawa Ally amewataka wanawake kutonyamazia vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa na waume zao majumbani.Mwadawa ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani ambayo kiwilaya yamefanyika katika kijiji cha Ngipa kata ya Engusero.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mwadawa amesema “ Kuna vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia ambavyo wanawake mnafanyiwa huko majumbani,lakini mnakaa kimnya, inawezekana wengine mnakaa kimnya kwa sababu hamfahamu kwamba kufanyiwa hivyo ni ukatili,au mnafahamu lakini mnaamua kunyamaza tu.Sio sahihi kunyamazia vitendo vya ukatili. Unapofanyiwa ukatili toa taarifa kwenye vyombo vya usalama ili wahusika wa vitendo hivyo wachukuliwe hatua stashiki.Kwa sababu kukaa kimnya kunatufanya wanawake tuendelee kuwa wanyonge kila siku.Tunajishughulisha sana kuinua uchumi wetu na wa familia zetu lakini bado tunaendelea kuwa wanyonge”.
Bibi Mwadawa ameelezea aina mbili za ukatili wa kijinsia ambapo aina ya kwanza ni ; wanawake wengi wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za kujitafutia kipato, lakini wanapopata pesa, waume zao huwanyang’anya pesa hizo na kuzitumia wao kwa matumizi yao binafsi.Na ya pili ni wanawake wanachukua mikopo kwa ajili ya biashara,lakini waume zao huchukua fedha hizo na kuzitumia kuolea,kupeleka kwa vimada ,kunywea pombe na kadhalika, hali ya kuwa wanawake hao ndio warejeshaji wa mikopo hiyo.Na pindi wanapojaribu kuhoji kuhusiana na vitendo hivyo huishia kupata vipigo.
Aidha Mwadawa amewataka wanawake kujitokeza, kujiunga kwenye vikundi na kufanya shughuli mbalimbali za ujasiliamali ili waweze kuondoa umaskini katika familia zao, kwa sababu uwezo wa kufanya hivyo wanao,kinachotakiwa ni kujiamini na kupambana kwa nguvu zote.Amesema kwamba jukwaa limeshazinduliwa tangu mwaka jana,lengo la jukwaa hilo ni kuwaunganisha wanawake kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali za kijasiliamali.sambamba na kuwatafutia fursa zitakazowawezesha kupanua shughuli zao ikiwemo mikopo kutoka katika taasisi kama mabenki,SACCOS na serikalini,hivyo ni vema wanawake wakahamasika kujiunga ili wainuke kiuchumi, watunze familia zao.
Wanawake wengi wamekuwa mstari wa mbele katika kufanya shughuli mbalimbali ili kujipatia kipato na kukuza uchumi wao. Pamoja na mwamko na bidii hiyo, wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali,ambapo changamoto hizo ndio chanzo cha wao kutokusonga mbele.Baadhi ya changamoto hizo hutokana na wanaume ambao bado wana mitazamo hasi kuhusu mwanamke.Humtazama mwanamke kama chombo cha kuzalisha mali,na mali zinapopatikana, mwenye mamlaka, sauti na haki ya umiliki wa mali hizo ni mwanaume.Mtazamo huo unawapa wanaume ujasiri wa kujimilikisha na kutumia kwa nguvu kila kitu kilichopo nyumbani, bila kujali kimepatikana vipi na kipo kwa malengo gani.
..........MWISHO..............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa