Watendaji wa Kata zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto wamehudhuria warsha iliyoandaliwa na Wizara ya Kilimo. Warsha hiyo ambayo imefanyika Julai 12,2024 katika Ukumbi wa Halmashauri ilikua na lengo la kuwapitisha watendaji hao kwenye vipengele muhimu vya Sheria Ndogo ya Kudhibiti Sumukuvu.
Akiongea katika warsha hiyo, Afisa Kilimo Mkuu kutoka Wizara ya Kilimo Ndg. Magreth Natai amesema kwamba kutokana na athari ambayo iliwakuta watanzania kutokana na sumukuvu, serikali iliona kuna haja ya kuwa na Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC).
Katika kukabiliana na madhara ya sumukuvu kitu cha kwanza ambacho mradi kilifanya ni kutoa mafunzo kwa wakulima na wadau wa mazao jinsi ya kuepukana na sumukuvu.
Mafunzo hayo yalijumuisha elimu mbalimbali ikiwepo kufuata taratibu zote za kilimo kuanzia kupanda kwa wakati, kuvuna kwa wakati na namna ya kuhifadhi mazao.
Aidha TANIPAC katika kudhibiti sumukuvu imeweza kujenga pia maghala pamoja na maabara.
Ndg. Natai ameongeza kwa kusema kwamba, baada ya mafunzo serikali iliona kuna haja ya kuja na sheria ndogo ambazo zimelenga kuhakikisha yale ambayo wakulima wamefundishwa wanayafuta.
Katika warsha hiyo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria (W), Wakili Chistopher Donald, amewapitisha watendaji hao kwenye vipengele vyote vya Sheria hiyo Ndogo ya Kuthibiti Sumukuvu lengo likiwa ni kuwajengea watendaji hao uwezo wa kwenda kusimamia sheria hiyo kwenye kata zao.
Nae Msimamizi wa mradi huo wilayani Kiteto Ndg. Balabala Pundugu amesema kwamba wilayani Kiteto mradi umeweza kufanya ujenzi wa ghala la kudhibiti sumukuvu pamoja na maabara. Ghala hilo ambalo lina uwezo wa kuchukua tani 2000 limejengwa katika kata ya Engusero.
Aidha Ndg. Pundugu ameongeza kwa kusema kwamba mradi pia umeweza kufanya uanzishaji wa mashamba ya mfano kwa wakulima 3000.
Mbali na hayo Mradi umeweza kutoa mafunzo kuhusu jinsi ya kudhibiti sumukuvu kwa makundi mbalimbali ikiwemo kwa wakulima, wataalamu wa kilimo, madiwani, wasindikaji, wasafirishaji na wafanyabiashara. Vilevile mafunzo hayo yalitolewa kwa viongozi wa Chama Tawala pamoja na kwa vijana mafundi ambao walipewa elimu ya kutengeneza vihenge vya chuma kwaajili ya kuhifadhia mazao.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa