Mbunge wa Jimbo la Kiteto, Mh. Edward Ole Lekaita, amefanya uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo ya Surua Rubella katika kata ya Sunya Februari 15, 2024.
Katika Kampeni hii ya Kitaifa ya siku nne kuanzia Februari 15-18, 2024, Halmashauri ya Wilaya Kiteto inalenga kuchanja watoto 57,435.
Chanjo ya Surua Rubella inatolewa bure kwa watoto walio na umri kuanzia miezi 9 hadi miezi 59 katika Hospitali ya Wilaya, Vituo vya Afya vyote, Zahanati zote na katika vituo maalumu vilivyoteluliwa kwa muda kutoa huduma hiyo. Kampeni hii ina lengo la kuongeza kinga kwa walengwa.
Surua ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa kwa njia ya hewa. Dalili za ugonjwa wa Surua ni pamoja na: Homa, mafua, Kikohozi, macho kuwa mekundu na kutoa majimaji; na vipele vidogo vidogo ambavyo huanza kwenye paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima
Rubella ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Rubella na kuenezwa kwa njia ya hewa. Mara nyingi huwapata watoto wadogo ingawa unaweza kumpata mtu wa umri wowote. Dalili zake hufanana na dalili za ugonjwa wa Surua.
Katika siku ya kwanza ya Kampeni hii ya uchanjaji Februari 15,2024, Wilaya ya Kiteto imeweza kuchanja watoto 14,584 na hivyo kuweza kufikia lengo la uchanjaji kwa siku ambapo lengo la siku lilikua kuchanja watoto 14,358.
Uzinduzi wa Kampeni hiyo uliambatana na zoezi la kukabidhi gari moja la wagonjwa (Ambulance) katika Kituo cha Afya cha Sunya. Uzinduzi huo wa chanjo pamoja na hafla ya kukabidhi gari hilo, mbali na kushuhudiwa na madiwani, wananchi na wataalamu kutoka katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, ulishuhudiwa pia na wabunge wawili ambao ni Mbunge wa Moshi Mjini Mh. Priscus Tarimo na Mbunge wa Msalala Mh. Kassim Idd.
Gari hilo lililokabidhiwa katika Kituo cha Afya Sunya ni kati ya magari mawili (2) ambayo sekta ya Afya katika Halmashauri ya Wilaya Kiteto ilipokea kutoka serikali kuu. Mwezi Desemba, 2023, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mh. Mohamed Mchengerwa alikabidhi magari 13 kwa mkoa wa Arusha na Manyara kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za Afya.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa