.........HABARI KAMILI ............
Kaimu katibu tawala wa wilaya ya Kiteto ndugu Fadhil Alexander amewaasa watumishi wilayani hapa kutofanya kazi kwa mazoea,.Alexander ameyasema hayo katika sherehe ya kuwaaga watumishi wa halmashauri waliostaafu mwaka 2018 pamoja na kuaga mwaka 2018 na kuukaribisha mwaka 2019 iliyofanyika katika ukumbi wa CCM uliopo katika mji mdogo wa Kibaya mwishoni mwa wiki.
Akizungumza wakati wa hotuba yake,Alexander ambaye amemuwakilisha Mkuuu wa wilaya ya Kiteto kama mgeni rasmi katika sherehe hiyo amesema “ Nawapongeza sana wazee wangu ninyi ambao utumishi wenu umefika ukomo.Ni ukweli usiopingika kwamba kwa muda wote mliokuwa katika utumishi mmekutana na majaribu ,vikwazo na changamoto mbalimbali lakini kwa sababu ya uadilifu,bidii na moyo wa kujituma mliweza kuyashinda yote na hatimaye kufikia kustaafu, na leo hii mnaagwa kwa heshima .Watumishi wote walioko hapa wanatakiwa kujifunza kitu kutoka kwenu,wasifanye kazi kwa mazoea,bali wawe waadilifu na wenye bidii na moyo wa kujituma”.
Katika sherehe hiyo pia timu ya mpira wa miguu ya watumish wilaya(Watumishi FC) ilipongezwa kwa kupata ushindi na kutawazwa kuwa bingwa wa mkoa wa Manyara katika mashindano ya ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa.Kufuatia ushindi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri alikuwa na haya ya kusema“hongereni sana kwa ushindi mlioupata.Ushindi tu ndicho kitu ambacho nilikuwa nakitamani kukisikia kutoka kwenu.Nimefurahi sana mmefanya kama nilivyokuwa natamani mfanye.Hii ndio timu sasa, na haya ndio mambo tunayoyataka.Ushindi huu unanipa moyo na nguvu ya kupambana kwa hali zote kuhakikisha kwamba mnaendelea mbele.Na ninyi sasa ni wajibu wenu kuongeza bidii kuhakikisha kwamba mnafanya vizuri zaidi mtakapokwenda ngazi ya taifa’’.
Baada ya pongezi hizo harambee fupi ilifanyika kwa lengo la kuiunga mkono timu hiyo ambapo fedha taslim kiasi cha sh. 776,500,na ahadi sh 1,540,000 zilipatikana.Aidha wastaafu wote walipewa zawadi.Na katika kuonyesha shukrani na furaha yao, wastaafu hao hawakuwa nyuma, walimshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kuwajali kiasi cha kuwaandalia sherehe ya kuwaaga, shukrani yao hiyo iliambatana na zawadi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.Baada ya matukio yote hayo kilichofuata ni kula na kunywa na kucheza muziki,ambapo watumishi wa taasisi mbalimba walijumuika pamoja katika kucheza muziki.
Halmashauri ya wilaya ya Kiteto imekuwa muandaaji wa sherehe hizo kwa miaka 3 mfululizo sasa, ambapo lengo lake kuu
ni kuwapongeza wastaafu kwa utumishi wao sambamba na kuwakutanisha watumishi wa taasisi mbalimbali za umma na za binafsi kukaa pamoja kufurahi na kushirikishana mawazo na uzoefu ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
..........MWISHO..............
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa