Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, CPA Hawa Abdul Hassan, Januari 20, 2025, ameongoza kikao maalum cha watumishi kujadili masuala ya uboreshaji wa mfumo wa kodi nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, CPA Hawa aliwasihi watumishi kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi. Maoni yaliyokusanywa yatapelekwa ngazi ya mkoa kupitia wajumbe wanne walioteuliwa wakati wa kikao hicho.
Watumishi walitoa mapendekezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa Kodi ya Ajira (PAYE) kwa watumishi wenye mshahara chini ya TZS 600,000, na kwa wale wenye mshahara zaidi ya kiwango hicho, kupunguza kiwango cha kodi hiyo kutoka 9% hadi 5%. Sambamba na hilo ni kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka 18% hadi 15%.
Aidha, watumishi hao walipendekeza kuanzishwa kwa Mfumo wa Makundi ya Kodi kwa watumishi ili kupunguza makali ya maisha. Hii ni pamoja na kuwapunguzia kodi watumishi wanaofungua biashara, kwa kuwa tayari wanakatwa kodi kwenye mishahara yao.
Watumishi pia walisisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya mlipakodi. Walibainisha kuwa idadi kubwa ya wananchi, wakiwemo watumishi, hawana uelewa wa kutosha kuhusu kodi wanazotozwa. Hivyo, walipendekeza kitengo cha Elimu ya Mlipakodi kiboreshwe ili kufanikisha utoaji wa elimu kwa makundi mengi zaidi ya wananchi.
Kuhusu Kodi ya Zuio (Withholding Tax), walishauri serikali irudishe jukumu la ukusanyaji kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuboresha ufanisi, kwa kuwa taasisi nyingine zinakabiliwa na changamoto za kiutekelezaji kutokana na miongozo iliyopo.
Aidha, watumishi walitoa maoni kuhusu mashine za kielektroniki (EFD). Walipendekeza serikali kutoa mashine hizo bure kwa wafanyabiashara waliokidhi vigezo, na kuweka utaratibu wa kukata gharama za mashine hizo kutoka kwenye Kodi ya Mapato ambayo hulipwa kila baada ya miezi mitatu. Pendekezo hili linalenga kuwasaidia wafanyabiashara ambao wanashindwa kumudu gharama za ununuzi wa mashine hizo.
Watumishi hao pia walipendekeza serikali ianzishe kipindi cha neema (grace period) cha miezi sita kwa watumishi wapya, ambapo hawatakatwa kodi. Walilinganisha hatua hii na neema inayotolewa kwa kampuni kubwa zinapoanza uwekezaji.
Mkurugenzi CPA Hawa Abdul Hassan, alitoa shukrani za dhati kwa watumishi kwa kushiriki kikamilifu na kuonyesha ari kubwa katika mjadala huo muhimu. Alisisitiza kuwa maoni yao ni ya thamani kubwa na yatasaidia kuleta mabadiliko chanya kwenye mfumo wa kodi nchini.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa