Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, SSI. Mbaraka Alhaji Batenga amewaomba wazee wilayani hapo kuisaidia serikali kukemea uporomokaji wa maadili katika jamii.
Ombi hilo limetolewa Oktoba 1,2023 katika Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Wilaya uliopo Kibaya wilayani hapo.
Mh. Batenga amesema kwamba utandawazi unawamaliza vijana ila wazee wakishirikiana na serikali na jamii kwa ujumla watafanikiwa kumaliza tatizo hilo.
“Kuna changamoto kubwa ya mporomoko wa maadili katika kizazi cha sasa hivyo nitoe ombi kwa wazee mtusaidie kusimamia na kukemea uporomokaji wa maadili”, alisema Mh. Batenga.
Aidha Mh. Batenga alitumia jukwaa hilo kuwaasa vijana kutimiza wajibu wao katika kuwatunza wazazi wao kama ambavyo wazazi hao walivyowajibika kuwatunza vijana hao.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya, Mh Abdallah Bundala, aliwasihi wazee hao kuzingatia mazoezi ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu.
Pia Mkurugenzi Mtendaji (W), CPA. Hawa Abdul Hassan, alisema kwamba ofisi yake ipo tayari muda wowote kwaajili ya kuwahudumia wazee hao hivyo endapo watakua na changamoto yoyote na wakashindwa kuhudumiwa ipasavyo katika ofisi zilizo chini yake, wanakaribishwa katika ofisi yake na atawasikiliza.
Nae Mganga Mkuu wa Wilaya, Dr. Vicent Gyunda, alisema kwamba, kwa kutambua changamoto za afya zinazowakabili wazee, kwa sasa hospitali ya wilaya imetenga madaktari wawili maalumu kwaajili ya kuwahudumia wazee tu ila katika vituo vya afya na zahanati hakuna madakatari waliotengwa kwaajili ya wazee hivyo huko utaratibu wa ‘mpishe mzee kwanza’ unatumika.
Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya alikabidhi kadi za bima ya afya ya jamii iliyoboroeshwa kwa wazee kumi ambao watahitajika pia kupeleka taarifa za wategemezi wao watano ili waweze kunufaika na huduma hiyo.
Maadhimisho hayo ambayo yalitanguliwa na matembezi ya hiyari, yalipambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo upimaji wa afya bure na michezo mbalimbali ambayo ilichezwa na wazee ikiwemo mchezo wa kukimbiza kuku, kuvuta kamba na maonesho ya mavazi na mchezo wa bao.
Katika zoezi la upimaji afya, wazee walipata fursa ya kupima macho na wale wote ambao walibainika na matatizo waliombwa kufika katika Hospitali ya Wilaya siku ya Terehe 10, Oktoba ,2023 kwaajili ya kupatiwa miwani. Aidha wazee hao walipata pia nafasi ya kupima shinikizo la damu, sukari, uzito na kupata ushauri mbalimbali wa afya kutoka kwa wataalamu wa afya wa wilayani hapo.
Akiongea kwa niaba ya wazee wengine, Mzee Habibu Hassan Surumbu alisema kwamba wamefurahi sana kuona uongozi wa wilaya mwaka huu umewathamini na kuwakumbuka kwenye siku yao hiyo muhimu kwa kuandaliwa maadhimisho hayo maana walikua wanaona tu kwenye vyombo vya habari wilaya nyingine zikifanya maadhimisho hayo.
Katika kufunga maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya aliwakumbusha wazee hao kuhusu mbizo za Mwenge wa Uhuru wilayani hapo na kuwahimiza kujitokeza katika mbio hizo.
Wilaya ya Kiteto inatarajia kuupokea Mwenge wa Uhuru Oktoba 7,2023 katika eneo la Dosidosi ambapo Mwenge huo wa Uhuru utakuwa ukipokelewa Kimkoa kutoka katika wilaya ya Kongwa iliyopo mkoani Dodoma.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa