Waziri wa OR- TAMISEMI Mh. Suleimani Jaffo akitoa maelekezo kuhusu mkandarasi aliyekuwa akifanya kazi ya ujenzi wa barabara KM 44 Kutoka namelock.
Waziri wa OR- TAMISEMI Mh. Suleiman Jaffo akikagua barabara ya Namelock - Sunya kama inavyoonekana katika picha
Waziri wa OR - TAMISEMI Mh.Suleimani Jaffo akielekea kukagua wodi ya wazazi katika kituo cha afya Sunya alipotembelea kituo hicho katika ziara yake wilayani Kiteto.
Waziri wa OR - TAMISEMI Mh.Suleimani Jaffo akikagua chumba cha kujifungulia katika kituo cha afya Sunya alipotembelea kituo hicho katika ziara yake wilayani Kiteto.Upande wake wa kulia ni mkuu wa wilaya ya Kiteto Mh. Tumaini Magessa.
Waziri wa OR - TAMISEMI Mh.Suleimani Jaffo akizungumza na wananchi wa Sunya katika mkutano wa hadhara katika ziara yake wilayani Kiteto
Wananchi wa kata ya Sunya wakimsikiliza Waziri wa OR - TAMISEMI Mh.Suleimani Jaffo
HABARI KAMILI....
Waziri Jaffo kuwashughulikia wakandarasi wababaishaji
Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI mheshimiwa Suleimani Jaffo ameahidi kuwashughulikia wakandarasi wababaishaji. Mheshimiwa Jaffo ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 88.1 ya Namelock - Sunya, ambapo alipokea taarifa ya kusitishwa kwa mkataba wa mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kilometa 44 kutoka namelock.Mheshimiwa Jaffo amesema kwamba pamoja na kusitisha mkataba wa mkandarasi huyo , ili kumsaidia kwa sababu ni mkandarasi Mtanzania, anatoa siku tano hadi tarehe 22 Novemba 2017, katika siku hizo, meneja wa TARURA Wilaya ya Kiteto amuite wakae nae waangalie kazi aliyoifanya, alipwe anachostahili waachane nae. Baada ya Jumatano kama atakuwa hajafika ,serikali itafanya utaratibu wa kumpeleka mahakamani kwani alikuwa na lengo la kuitapeli serikali kwa sababu alishakiuka mkataba kwa kushindwa kutimiza vigezo vinavyotakiwa kama vilivyoainishwa kwenye mkataba ikiwemo kuleta dhamana ya utendaji kazi. Mheshimiwa Jaffo amesisitiza kuwa katika ofisi yake wakandarasi kama hao hawataki kabisa, hivyo kama mkandarasi huyo atakuwa hajatekeleza alichoagiza, jina la mkandarasi huyo lipelekwe ofisini kwake , na atahakikisha kwamba hapati kazi yoyote ya TARURA katika jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Aidha Mheshimiwa Jaffo amesema kwamba ameridhishwa na hatua ilyochukuliwa na meneja wa TARURA wilaya ya Kiteto mhandisi Gerald Matindi ya kusitisha mkataba wa mkandarasi huyo kwa sababu ameshindwa kufanya kazi hiyo kwa kasi na kiwango kinachotakiwa, kwani amefanya kazi kwa asilimia saba ambapo ni kilometa kumi na saba tu kati ya kilometa 44, tangu ameanza kazi hiyo tarehe 17/06/2017.Vilevile mheshimiwa Jaffo amemsifu mkandarasi anayejenga barabara hiyo kilometa 44.1 baada ya Namelock, ambapo amesema kwamba mkandarasi huyo yuko vizuri sana, Kazi yake ni nzuri na kasi ya utendaji kazi wake ni ya kuridhisha.
Nae mtendaji mkuu wa TARURA Tanzania mhandisi Victor Seif amesema kwamba wakandarasi wa aina hiyo kama watakuja kuomba kazi hawana uwezo hawatawavumilia kabisa, hata katika tathmini.Na ikitokea kwamba wameleta vigezo ambavyo sio vya kweli wakapewa kazi ,wakati wa kutekeleza kazi hizo kama hawatafanya vizuri TARURA itasitisha mikataba yao. Mhandisi Seif anasema ‘‘Mkandarasi huyu hatapewa tena kazi ya kiwango hiki, hadi atakapotuhakikishia kuwa anavifaa vya kutosha na wataalamu wa kutosha kusimamia kazi ya ukubwa huu .Pia Maagizo ya mheshimiwa waziri tumeyapokea,mkandarasi huyu tutamuita tutaangalia kazi aliyofanya , kama kuna kitu anadai tutamlipa ili tuachane nae, akikaidi tutaanza taratibu za kumuweka kwenye orodha ya wakandarasi ambao hatutawapa kazi tena ,tutaanza taratibu hizo kwa sababu anayetakiwa kufanya hivyo ni PPRA”.
Katika hatua nyingine mheshimiwa Jaffo ametembelea Kituo cha afya cha Sunya ambapo amekagua wodi ya wazazi na chumba cha kujifungulia, baada ya kuona hali halisi ya ya kituo hicho, amemuagiza kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Emmanuel Mwagala kuwa kufikia ijumaa ya tarehe 24/11/2017 ujenzi wa wodi ya wazazi,chumba cha upasuaji,maabara na chumba cha kuhifadhia maiti katika kituo hicho uwe umeanza .Vilevile amezungumza na wananchi wa kata ya Sunya katika mkutano wa hadhara , ambapo amesisitiza juu ya usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya maendeleo hususani barabara na ushirikishwaji wa wananchi katika miradi hiyo ili iweze kutekelezwa kwa ufanisi . Katika mkutano huo mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amemueleza mheshimiwa waziri kuhusu migogoro ya mipaka kati ya wilaya ya Kiteto na Kilindi. Pia mbunge wa jimbo la Kiteto mheshimiwa Emmanuel Papian alieleza kero za wananchi wa Sunya, kero kubwa ikiwa ni msitu wa SULEDO na uongozi wa SULEDO ,ambapo wananchi walionyesha dhahili kuguswa sana na kero hiyo , hapa mheshimiwa Jaffo anatoa tamko anasema ‘‘Nitaunda timu maalumu kuja kushughulikia jambo hili, timu hiyo nitakayoiunda nitawapa hadidu rejea kubaini hizo fedha zinazokusanywa zinaenda wapi?Tusivumilie hii tabia ya wananchi wanakuwa na malalamiko siku zote. Leo mimi nimepokelewa na mabango, kesho Rais wangu atakuja atapokelewa na mabango, lazima tuchunguze kuna nini hapo? Nini chanzo cha tatizo? Kama mmeuhifadhi msitu , na nimesikia kuwa mna katiba yenu, na bila shaka mna taratibu zenu,nadhani mna malengo mahususi na msitu huo, sasa kama kuna watu wamejimilikisha msitu huo ,tutaangalia taratibu baada ya timu hiyo kumaliza kazi yake. Kama kuna wezi ,utaratibu wa wezi unajulikana ni kufikishwa katika vyombo vya sheria”. Kuhusu migogoro ya mipaka kati ya Kilindi na Kiteto, mheshimiwa Jaffo amesema kwamba watalifanyia kazi suala hilo ili lifike mwisho .
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa