Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Nape Moses Nnauye, ameuagiza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambao upo chini ya wizara yake, kujenga mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Makame wilayani Kiteto..
Maagizo hayo ameyatoa Mei 13, 2024 katika kijiji cha Kinua kilichopo kata ya Namelock katika Wilaya ya Kiteto kwenye ziara yake ya kukagua upatikanaji wa huduma ya mawasiliano kijijini hapo.
Upatikanaji wa mawasiliano katika kijiji cha Kinua umekuja baada ya kujengwa na kuwashwa kwa mnara wa Airtel ambao umejengwa kwa ubia pamoja na UCSAF, mfuko ambao una jukumu la kupeleka mawasiliano kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara kwa makampuni ya simu.
Akiongea na wananchi katika kijiji cha Kinua mara baada ya kumaliza kukagua mnara huo, Mh. Nape amewaambiwa wananchi hao kua upatikanaji wa mawasiliano katika kijiji hicho ni juhudi pia za mbunge wa Jimbo la Kiteto Mh. Edward Olelekaita ingawa kijiji cha Makame ambapo anatokea Mbunge huyo hakuna huduma ya mawasiliano ila Mbunge huyo hakua mbinafsi wala hakutaka kujipendelea. Kutokana na moyo huo wa kizalendo na upendo wa Mbunge huyo, Mh. Nape ameiagiza UCSAF kuhakikisha mnara unajengwa katika kijiji hicho cha Makame.
Aidha Mh. Nape amesema kwamba serikali imepeleka mawasiliano kwasababu dunia ya leo mawasiliano ni haki ya binadamu hivyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapa wananchi haki hiyo.
Vilevile aliongeza kwa kusema kwamba katika Kijiji cha Kinua hakuna huduma za kibenki ndio maana wakajengewa mnara ili kuwezesha kuwasiliana na kuwawezesha kupata huduma za kibenki.
“Tunapoenda, huduma nyingi za serikali zitawekwa kwenye mitandao mfano tumeanza majaribio ya kuomba barua ya utambulisho. Huduma nyingi zitaongezwa kwahiyo ndugu zangu tumewaletea maisha kwani mawasiliano ni maisha”, ameongeza Mh. Nape.
Mh. Nape ameipongeza UCSAF na pia aliishukuru kampuni ya simu ya Airtel kwa kuwawezesha wananchi wa kijiji hicho kupata mawasiliano.
Aidha aliwaasa wananchi wa kijiji hicho kuhakikisha wanalinda miundombinu ya mawasiliano kwani inajengwa kwa gharama kubwa na imejengwa kwa manufaa yao wananchi.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa