Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo akisaini kitabu cha wageni katika ikulu ndogo ya Kibaya mara baada ya kuwasili wilayani Kiteto
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mhe. Tumaini Magessa akiwasilisha taarifa fupi ya ujenzi wa jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Kiteto kwa waziri wa TAMISEMI Mhe.Suleiman Jaffo
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo akikagua mradi wa ujenzi wa jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Kiteto
Waziri wa TAMISEMI Mhe.Suleiman Jaffo akitoa maelekezo kuhusu mradi wa ujenzi wa Barabara ya Nameloku - Sunya
Mkuu wa shule ya sekondari Engusero akimkaribisha waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo alipotembelea shuleni hapo katika ziara yake wilayani Kiteto
Wanafunzi wa shule ya sekondari Engusero wakiwa wamekusanyika kumsikiliza waziri wa TAMISEMI mhe. Suleiman Jaffo alipotembelea shuleni hapo katika ziara yake wilayani Kiteto
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo akiwa katika picha ya pamoja na wasichana wanaosoma kidato cha tano katika shule ya sekondari Engusero
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo akiwa katika picha ya pamoja na wavulana wanaosoma kidato cha tano katika shule ya sekondari Engusero
Watumishi wa Kituo cha afya cha Engusero wakimkaribisha waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo alipotembelea kituo hicho katika ziara yake wilayani Kiteto
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo akiingia katika kituo cha afya cha Engusero kuona hali ya kituo hicho katika ziara yake wilayani Kiteto
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Jaffo akizungumza na wakazi wa kata ya Engusero baada ya kukagua miradi katika ziara yake wilayani kiteto
Wakazi wa kata ya Engusero wakiwa wamekusanyika kumsikiliza waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jaffo
HABARI KAMILI...
Waziri wa TAMISEMI afanya ziara wilayani Kiteto
Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mheshimiwa Suleiman Jaffo amefanya ziara wilayani Kiteto mkoa wa Manyara.Katika ziara hiyo Mhe. Jaffo amekagua mradi wa ujenzi wa jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Kiteto, ujenzi wa barabara ya Nameloku – Sunya, ametembelea shule ya sekondari ya Engusero pamoja na kituo cha afya cha Engusero, na kuzungumza na wakazi wa kata ya Engusero .
Akiwasilisha taarifa fupi ya mradi wa ujenzi wa jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Kiteto kwa waziri wa TAMISEMI mheshimiwa Suleiman Jaffo, mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amesema kwamba jengo hilo lilianza kujengwa tarehe 26/10/2016 na kwamba hatua ya ujenzi huo ni ya kuridhisha , aidha mheshimiwa Magessa amemueleza mheshimiwa Jaffo kuwa mkandarasi yuko nyuma ya muda kutokana na kucheleweshewa fedha za mradi huo, na kwamba kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 3.4 kimebaki ili kukamilisha mradi huo. Jengo hilo la gorofa mbili hadi kukamilika kwake litagharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 4.5.
Akikagua mradi huo wa ujenzi wa jengo jipya la halmashauri , mheshimiwa Jaffo amesema kwamba ameridhika na kazi iliyofanyika na kumpongeza mkandarasi kwa kazi nzuri, mheshimiwa Jaffo ameisifu kampuni inayojenga jengo hilo, ambapo amesema kwamba kampuni hiyo ni ya kizalendo lakini inafanya vizuri sana, aidha amemuahidi mkandarasi kuwa fedha zitapatikana,wala wasihofu anachotaka ni kazi ikamilike. Mheshimiwa Jaffo pia amemuagiza afisa ardhi kuhakikisha kuwa eneo hilo linapimwa na linapata hati ili kuzuia migogoro baina ya serikali na wananchi wa eneo hilo .
Katika ukaguzi wa mradi wa barabara, mheshimiwa Jaffo amesema kwamba hajaridhika na kasi ya mkandarasi anayetengeneza barabara hiyo kutoka Nameloku. Akijibu hoja hiyo ya mheshimiwa waziri meneja wa TARURA wilaya ya Kiteto mhandisi Gerald Matindi amesema kwamba wameshakaa kikao cha juu cha menejimenti kumjadili na wanalengo la kukatisha mkataba wake, isipokuwa ameomba wiki moja menejimenti iangalie utendaji wake kama wataridhika au la.Wakishaangalia kama hatakuwa amefanya kazi kiasi cha kuridhisha , mshauri wao ataanza taratibu za kusitisha mkataba wa mkandarasi huyo. Pamoja na majibu ya meneja huyo wa TARURA mheshimiwa Jaffo anatoa angalizo kwa meneja wa huyo anasema “Tumeanzisha wakala wa TARURA , lengo kubwa ni kwamba barabara zitengenezwe kwa uhakika zaidi, na tumekuteua wewe meneja ukae hapa lengo ni kwamba usifikirie jengo, usifikirie choo kimebomoka ,usifikirie darasa halipo, lengo lako ukiamka asubuhi unafikiria jinsi gani barabara ziimarike . Ndio maana kubwa ya kuweka wakala wa TARURA. Jambo la pili tunataka wakandarasi ambao walikuwa wakifanya kazi kimazoea , katika utaratibu wa sasa hivi wasiwepo. Tunataka barabara zenye ubora.Kwa namna ambavyo mmeshasukumana nae ,hadi kufikia hatua ya kutakaka kusitisha mkataba wake, mimi napata mashaka kama mkandarasi huyu ataweza kujenga barabara hii kwa kiwango kinachotakiwa. Angalieni uwezo wa huyu mkandarasi je unatosha? tusiwe na mtu ambae ataharibu barabara zetu. Muangalieni kama hana uwezo fukuza”. Kutokana na kutoridhishwa na kasi mradi huo wa ujenzi wa barabara , mheshimiwa Jaffo ameahidi kurudi Kiteto tarehe 17 /11 kwa ajili ya kukagua barabara hiyo ili kuona kazi imefika wapi,na kama haijafanyika atataka kujua ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya mkandarasi huyo. Mradi huo wa Barabara ya Nameloku – Sunya una kilomita 88.1 , hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 6.4.
Vilevile mheshimiwa Jaffo alitembelea shule ya sekondari Engusero. Katika shule ya Sekondari Engusero mheshimiwa Jaffo amekagua madarasa mapya mawili yaliyojengwa na halmashauri pamoja na bweni la wasichana, ambapo ameupongeza uongozi wa wilaya ya Kiteto kwa juhudi kubwa waliyoifanya kuhakikisha kuwa wanakuwa na shule mbili za kidato cha tano , pia amewapongeza walimu wa shule hiyo kwa kazi kubwa wanayofanya. Aidha mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa alimweleza waziri kuwa wamefanikiwa kujenga madarasa mawili na mabweni mawili kwa ajili ya kidato cha tano, mwakani wanafunzi hao waliopo kidato cha tano wataingia kidato cha sita, wanafunzi wengine wa kidato cha tano watakuja,hawatakuwa na mahali pa kuwalaza. Nae Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mheshimiwa Lairumbe Mollel alimuomba mheshimiwa waziri kwamba serikali iwaunge mkono katika kusaidia kukamilisha miradi ambayo wao kama halmashauri wamekuwa wakiianzisha kwa kutumia fedha za ndani, ambapo mheshimiwa Jaffo aliahidi kuwaunga mkono kwa kuongeza madarasa mawili ,mabweni mawili pamoja na vyoo . Mheshimiwa Jaffo pia alizungumza na wanafunzi wanaokaa bweni katika shule hiyo na kuwaasa kuzingatia masomo na kutokujiingiza katika mambo yasiyowahusu, mambo ambayo yataharibu mustakabali wa elimu yao na maisha yao kwa ujumla. Pia mheshimiwa Jaffo aliwapongeza wanafunzi hao kwa kuweka mazingira yao ya shule vizuri na kuwaahidi kuwa serikali itafanya kila liwezekanalo kuboresha mazingira ya shule hiyo ili vijana wanaochaguliwa kujiunga na shule hiyo waweze kusoma vizuri. Mheshimiwa Jaffo aliwaeleza wanafuzi hao kwamba ameshaahidi kuongeza madarasa mawili, mabweni mawili, matundu ya vyoo ,na kama uwezekano upo bwalo la chakula ambalo liko katika hatua ya lenta limaliziwe na pia wajengewe jiko zuri,kwani ameona jiko linalotumika shuleni hapo lina hali mbaya,halistahili kutumika kupika chakula cha watoto hao.
Aidha mheshimiwa Jaffo alitembelea kituo cha afya cha Engusero ambapo alikagua stoo ya kuhifadhia madawa, wodi na jengo la upasuaji. Akiwa kituoni hapo ,mheshimiwa Jaffo alielezwa kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo watumishi katika kituo hicho, changamoto hizo ni uhaba wa baadhi ya dawa, kutokuwepo kwa chumba cha upasuaji kutokana na chumba kilichopo kuthibitishwa na wataalamu baada ya ukaguzi kutokufikia kiwango cha kutumika kwa upasuaji, kutokuwepo kwa wodi ya kina mama ambao wanangojea kujifungua na ambao wameshajifungua, hali inayosababisha wakina mama hao kuchanganyika na wagonjwa wengine .Baada ya kusikia changamoto hizo mheshimiwa Jaffo ameahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga chumba cha upasuaji cha kisasa , kuongeza wodi ya kina mama wanaongojea kujifungua na wodi ya wakina mama waliojifungua,na kuleta vifaa vyote vinavyohitajika ili kituo hicho kiweze kuwahudumia wakazi wa Engusero kwa ubora zaidi.
Mheshimiwa Jaffo alihitimisha ziara yake wilayani Kiteto kwa mkutano wa hazara ambapo alizungumza na wakazi wa kata ya Engusero. Mheshimiwa Jaffo aliwaeleza wananchi kuwa ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Magufuli amesimamia kidete kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi zinalindwa kwa nguvu zote.Raisi anapambana kuboresha maisha ya watanzania, hali ya afya ilikuwa mbaya,bajeti ya afya ilikuwa duni sana,Rais ameongeza bajeti ya madawa kutoka bilioni thelasini na moja kwa mwaka hadi bilioni mia mbili sitini na tisa kwa mwaka.Hali ya vituo vya afya ilikuwa duni , Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli inajenga vituo vya afya 172, na wilaya ya kiteto ni miongoni mwa wilaya zilizopo katika mpango wa kujengewa vituo vya afya ambapo imeshaingiziwa shilingi milioni mia nne kwa ajili ya kujenga kituo cha afya cha Sunya. Mheshimiwa Jafo anasema “Licha ya kwamba tumeleta fedha katika kituo cha Sunya,na zitakuja fedha nyingine shilingi milioni mia tatu na ishirini, huko Sunya, kituo kikikamilika tutaleta vifaa vyote. Lakini nimefika katika kituo chenu cha afya hapa nimegundua na hapa kuna changamoto kubwa sana.Kwa uwezo wa Mungu ,sio kwa uwezo wangu,Mungu akijalia nitaleta fedha tutajenga jengo la upasuaji la kisasa hapa ,tutajenga wodi ya wazazi, tutajenga jengo la kuhifadhia maiti ili mtu akifariki ahifadhiwe hapahapa ”.
Naye mbunge wa Kiteto mheshimiwa Emmanuel Papian mbele ya wananchi wa Engusero waliokusanyika ili kumsikiliza mheshimiwa waziri akatumia fursa hiyo kuwasilisha kero za wananchi wa Kiteto kwa mheshimiwa waziri, mheshimiwa Papian anasema “Wilaya ya kiteto ina tatizo la uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali , mheshimiwa waziri naomba katika ajira zitakazotoka uitazame wilaya ya Kiteto kwa jicho la huruma, wilaya ya Kiteto ikumbukwe kwa kuletewa watumishi ambao watakuja kuchapa kazi .Pia tuna tatizo la maji nakuomba mheshimiwa waziri kupitia wizara yako ya TAMISEMI kitengo cha maji utusaidie kupata maji.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa