Afisa elimu msingi ( W) Ndg. Emmanuel Mwagala akizungumza kuhusu matokeo ya darasa la saba ofisini kwake mapema leo.
HABARI KAMILI
Afisa Elimu msingi wilaya ya Kiteto ndugu Emmanuel Mwagala amewapongeza walimu wa shule za msingi wilayani hapa kwa jitihada walizozifanya katika ufundishaji ,ambapo kupitia jitihada hizo , katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba mwaka 2018 kiwango cha ufaulu kimeongezeka.Mwagala ameyasema hayo katika mahojiano mafupi yaliyofanyika ofisini kwake mapema leo.
Akizungumza wakati wa mahojiano hayo Mwagala amesema “Matokeo ni mazuri sana yametutia moyo,walimu wamefanya kazi . Pamoja na mazingira magumu , lakini tumeweza kupata ufaulu wa asilimia 69.5, kwa wilaya kama hii yenye changamoto nyingi,huo ni ufaulu mzuri,lakini pia lengo letu ni kufanya vizuri zaidi, na tunaamini kwamba hilo linawezekana”.
Mwagala amefafanua zaidi kuhusu kiwango hicho cha ufaulu hapa anasema “Jambo lingine ambalo limetufurahisha ni kwamba wilaya yetu imetoa shule bora, katika shule ambazo zina watahiniwa zaidi ya 40,shule ya msingi Boma imekuwa ya kwanza kimkoa , si hivyo tu bali katika kundi hilo la shule zenye watahiniwa zaidi ya 40 shule hiyo imeshika nafasi 54 kitaifa jambo ambalo ni la kujivunia sana”.
Kadhakika Mwagala amesema kwamba kuna mabadiliko makubwa sana katika viwango vya ufaulu kwa mwaka 2018 ikilinganishwa na mwaka 2017 , ambapo mwaka huu 2018 , kwa ufaulu wa wastani wa GPA, kati ya shule 88 ni shule moja tu ambayo haijafikia watani wa 50, tofauti na mwaka 2017 ambapo shule zaidi ya 30 zilikuwa na wastani chini ya 50.
Naye Katibu tawala wa Mkoa wa Manyara ndugu Musa Musaile katika kikao chake na wakuu wa idara na vitengo wakati wa ziara yake wilayani hapa mwishoni mwa wiki ameipongeza sana wilaya ya Kiteto kwa ufaulu huo ambapo amesema kwamba Kiteto imejitahidi sana kwa shule zake nyingi kuwa na ufaulu kwa zaidi ya 50%.Na kwamba shule iliyoshika nafasi ya kwanza kimkoa ni kutoka wilaya ya Kiteto.
Mwagala pia amesema kwamba idara yake imejipanga kuhakikisha kwamba kiwango cha ufaulu kinaendele kupanda mwaka hadi mwaka, na ili kufanikisha hilo iko mikakati ambayo wameiweka ambayo itawawezesha kutimiza lengo hilo.
Mwagala ameiainisha mikakati hiyo, mkakati wa kwanza ukiwa ni kuwapa motisha walimu kwa kuwapongeza,kuwapa zawadi na kutambua kazi waliyoifanya ili waweze kujituma zaidi , mkakati wa pili ni kuanza maandalizi mwezi Januari mara tu shule zinapofunguliwa,kwa kuwapa wanafunzi wa darasa la saba mazoezi kwa wingi, mitihani kwa wingi, mkakati wa tatu ni kuwajengea walimu uwelewa zaidi katika mada wanazofundisha ili waweze kuwafundisha wanafunzi vizuri, na wanafunzi waweze kuelewa na mkakati wa nne ni kufanya ufuatiliaji wa karibu kila mara ili kuhakikisha kwamba walimu wanafundisha kulingana na maelekezo na malengo ambayo wilaya imejiwekea.
.....MWISHO.....
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa