Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mhe. Lairumbe Mollel akizungumza wakati akifungua kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika oktoba 30 -31 katika ukumbi wa halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Ndg. Tamim Kambona akizungumza wakati wa kikao cha baraza la madiwani.
Baadhi ya madiwani wakiwasilisha taarifa za kata zao katika kikao cha baraza la madiwani.
Waheshimiwa madiwani , wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ,wageni wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani .
............HABARI KAMILI...........
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto mheshimiwa Lairumbe amewapongeza na kuwashukuru walimu pamoja idara ya elimu chini ya Mkurugenzi ,kwa kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba,hali iliyosababisha ongezeko la ufaulu la 10.54 % .Amesema kwamba kiwango hicho cha ufaulu kinaonyesha kuwa wilaya inasonga mbele.Mheshimiwa Mollel ametoa pongezi na shukrani hizo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, Oktoba 30, mwaka huu.
Akizungumza kuhusu kiwango cha ufaulu Mheshimiwa Mollel amesema kwamba katika mwaka huu 2018 ,ufaulu wa wilaya ya Kiteto umekuwa ni 69.55% , wakati mwaka jana 2017 ilikuwa ni 59.01 % .Akionyesha kufurahishwa na kiwango hicho cha ufaulu , Mhe. Mollel amesema “Katika shule ambazo zimefanya vizuri,shule ya msingi Boma imeshika nafasi ya kwanza kimkoa, na imeshika nafasi ya 54 kitaifa, shule hiyo moja imetutoa kimasomaso. Shule kushika nafasi ya 54 katika shule zaidi ya 10,000 sio jambo dogo,ni jambo kubwa sana. Walimu wamefanya kazi nzuri sana”.
Mhe. Mollel amezitaja kata ambazo ziko katika kumi bora kwa ufaulu,ambapo amesema, kata ya kwanza ni Kaloleni,kata ya pili ni Partimbo,kata ya tatu ni Ndedo,kata ya nne Magungu,ya tano ni Bwagamoyo ,ya sita ni Matui, ya saba ni Kibaya . Ya nane ni Chapakazi, ya tisa ni Kijungu na ya kumi ni Ndirigishi .
Kadhalika Mhe Mollel amesema kwamba kwa sababu ufaulu unaonekana uko vizuri,wao kama madiwani wahakikishe kwamba wanafunzi waliofaulu wanapata madarasa na viti vya kukaa.Isije ikatokea kwamba watoto wameshindwa kwenda shule kwa sababu ya ukosefu wa vyumba vya madarasa.Ameongeza kwamba Mkurugenzi ana sehemu yake, lakini wao kama wazazi ,na wenyeviti wa ODC lazima wahakikishe kwamba wanafunzi waliofaulu wanakwenda shule.
Aidha Mhe. Mollel amewataka Wahe. madiwani kwenda kujipanga kuhakikisha kwamba wanafunzi watakaopangiwa kwenye kata zao, wote wanakwenda shule.Sambamba na hayo amewahimiza kwenda kujipanga vema kutoa zawadi kwa walimu wa shule zilizofanya vizuri ili kuwatia moyo kufanya vizuri zaidi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto ndugu Tamim Kambona amesema kwamba wamepanga mikakati ili kuhakikikisha kwamba wanaendelea kuboresha elimu katika wilaya hii; mikakati hiyo ni kuimarisha ushirikiano kati ya walimu,wazazi na wanafunzi, kuwatembelea walimu na wanafunzi kila wakati,kuhakikisha ufundishaji unafanyika vizuri,vile vile wameendelea kutoa motisha,kwa shule ambazo zimekuwa zikifanya vizuri.Na kwamba shule ya msingi Boma ambayo imekuwa ya kwanza kimkoa mwaka huu wanawatafutia zawadi kubwa zaidi ya ile waliyowapa shule ya msingi Laalakir ambayo ilishika nafasi ya kwanza mwaka 2017, ambapo wanaamini kwamba kwa kufanya hivyo wanazipa changamoto shule hizo kuongeza jitihada ili ziweze kufanya vizuri zaidi. Pia wameendelea kuhamasisha utoaji wa vyakula shuleni,na kwamba huo ndio msimamo wao, kuhakikisha wazazi wanachangia vyakula mashuleni, watoto wapate chakula shuleni wasome vizuri,kiwango cha ufaulu kiongezeke zaidi.
Katika hatua nyingine diwani wa kata ya Partimbo Mhe. Paulo Tunyoni amesema kwamba ili kuinua kiwango cha elimu wazee watano wa jamii ya kifugaji kutoka katika kitongoji cha Nabirikunya wameamua kujenga shule kwa kutumia mifugo yao,na kwamba hadi sasa wazee hao wameshachanga kiasi cha shilingi 13,500,000/= ,ambapo kazi ya ujenzi wa madarasa pamoja na ofisi za walimu itaanza mnamo tarehe 02/11/2018 .
Idara ya elimu msingi na idara ya elimu sekondari wilaya ya Kiteto, chini ya uongozi na usimamizi makini wa Mkurugenzi Mtendaji Tamim Kambona imekuwa ikifanya jitihada za makusidi kuhakikisha kwamba ,inaboresha elimu, inainua taaluma na kuongeza kiwango cha ufaulu mwaka hadi mwaka.
.......MWISHO..........
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa