Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Makame (WMA Makame), imeingia mkataba mpya wenye thamani ya shilingi bilioni 10 na kampuni iitwayo UNTAMED Horizons Camps & Safaris LTD.
Mkataba huo umesainiwa Novemba 18, 2023 katika Ofisi za Jumuiya zilizopo katika kijiji cha Makame huku ukishuhudiwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali wilayani hapo.
Akiongea katika tukio hilo, Mwenyekiti ya Halmashauri ya Wilaya Kiteto, Mh. Abdala Bundala amewakaribisha wawekezaji hao na kuahidi kuwapa ushirikiano kwani wanatambua na wanaona matokeo ya uhifadhi kwenye Halmashauri yake.
Nae Mkurugenzi Mtendaji (W), CPA. Hawa Abdul Hassan,amesema kwamba anatambua umuhimu wa utalii katika Halmashauri hususani katika kuchangia mapato ya Halmashauri na kusema kwamba kutokana na shughuli za utalii katika hifadhi hiyo, taarafa ya Makame imekua na uhakika wa upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika hafla hiyo ya kusaini mkataba, kampuni ya UNTAMED pia imekabidhi gari aina ya Land Cruiser Hard Top lenye thamani ya shilingii milioni 150 kwa ofisi za WMA Makame pamoja na pikipiki mbili kwaajili ya kusaidia shughuli za doria katika hifadhi hiyo. Pamoja na hayo kampuni hiyo imekadhi kompyuta mpakato moja pamoja na printa mashine moja kwaajili ya ofisi ya WMA Makame
Mkataba huo umekua na neema kwa wananchi katika vijiji vya jumuiya hiyo kwani Kampuni ya UNTAMED pia imeahidi kutoa Bima ya Afya kwa wazee 100 kutoka katika vijiji hivyo pamoja na kuchimba visima vitano (kila kijiji kisima kimoja) vya maji ambavyo vitaendeshwa kwa nishati ya jua.
Aidha, kampuni hiyo imeahidi kuchimba mabwawa mawili na imeahidi kufungua barabara kwa urefu kwa takribani km 100 ili kuunganisha vijiji hivyo
Nae Mbunge wa Jimbo hilo Mh Edward Olelekaita, aliisihi Kampuni hiyo kutekeleza ahadi kama walivyoahidi na pia kuwasihi kufanya kazi na jumuiya na sio mtu mmoja mmoja.
Pia Mkuu wa Wilaya Kiteto,SSI. Mbaraka Batenga ambaye ndiye alikua Mgeni rasmi katika hafla hiyo, mbali na kuwakaribisha wawekezaji hao alisema kwamba anafahamu Kampuni hiyo inafanya biashara nyingine ikiwemo biashara ya vituo vya mafuta na vifaa vya ujenzi. Vilevile aliialika Kampuni hiyo kufika na kuwekeza katika biashara ya Vituo vya Mafuta kwakua Kiteto bado inauhitaji wa kupata msambazaji mkubwa wa mafuta.
WMA Makame ambayo inaundwa na vijiji vitano, imeingia mkataba na kampuni hiyo kwaajili ya shughuli za uwindaji katika kitalu cha Masai East. Vijiji vinavyounda WMA Makame ni Makame, Ndedo, Ngaboro, Katikati na Irkiushiobor.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa