Katika hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha elimu nchini, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, ameongoza kikao maalum cha kutambulisha miradi yenye thamani ya zaidi ya bilioni 1.8 kwaajili ya shule 11 wilayani hapa.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Julai 24, 2025, Mhe. Mwema alisema fedha hizo za program.ya BOOST kutoka Serikali Kuu chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kielelezo cha upendo kwa wana Kiteto, na aliahidi kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa umakini ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na katika ubora wa hali ya juu.
"Kwasababu miradi hii ina jicho la tatu, watu wote wanaohusika kwenye mifumo naomba msimamie vizuri, nasisitiza sana mkasimamie vizuri," alisema kwa msisitizo Mhe. Mwema.
Aliitaka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuweka mpango thabiti wa usimamizi, ukadiriaji sahihi wa vifaa. Vilevile kwa wasimamizi wa miradi ngazi ya chini aliwasisitiza kuwa makini na uteuzi wa wazabuni na mafundi. Alionya dhidi ya kuwatumia wazabuni na mafundi wasio na uwezo, akisema mara nyingi wamekuwa chanzo cha ucheleweshaji wa miradi.
Katika kikao hicho, Afisa kutoka TAKUKURU, Ndg. EliBrighton Mmari alisisitiza wajumbe wote kuwa waaminifu na waadilifu, akibainisha kuwa taasisi hiyo itasimama bega kwa bega na halmashauri kuhakikisha hakuna mianya ya rushwa katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Kikao hicho kilihudhuriwa na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, viongozi wa Chama na Serikali na watendaji wa vijiji na kata kutoka sehemu ambazo miradi hiyo itatekelezwa.
Fedha za kutekeleza miradi hiyo ambayo ni shilingi 1,881,000,000 zimekwisha kuingizwa kwenye akaunti za shule hizo toka wiki ya kwanza ya Julai 2025.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa