Ng'ombe anavyoonekana baada ya kupigwa chapa katika zoezi la upigaji chapa ng'ombe lililozinduliwa katika kata ya Namelock wilayani Kiteto tarehe 24/11/2017
Ng'ombe wakisubiri kupigwa chapa katika uzinduzi wa zoezi la upigaji chapa wilayani Kiteto
Viongozi wa wilaya ya Kiteto wakisubiri uzinduzi wa zoezi la upigaji chapa ngombe wilayani Kiteto
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mh. Tumaini Magessa akizungumza kuhusu zoezi la upigaji chapa ngombe
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mh. Hassani Benzi akizungumza kuhusu zoezi la upigaji chapa ng'ombe
Diwani wa kata ya Partimbo Mh. Paulo Tunyoni akizungumza kuhusu zoezi la upigaji chapa ngombe wilayani Kiteto
Afisa mifugo wilaya ya Kiteto ndugu William Msuya akizungumza kuhusu zoezi la upigaji chapa ngombe
Kiongozi wa mila kutoka jamii ya Wafugaji wanaoishi wilayani Kiteto ndugu Ngayoni Lebakari akizungumza kuhusu zoezi la upigaji chapa ngombe
Mkuu wa wilaya ya Kiteto Mh. Tumaini Magessa akipiga chapa ng'ombe katika uzinduzi wa zoezi la upigaji chapa ng'ombe wilayani Kiteto
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto Mh. Hassan Benzi akipiga chapa ng'ombe katika uzinduzi wa zoezi la upigaji chapa ng'ombe wilayani Kiteto
Afisa mifugo wilaya ya Kiteto ndugu William Msuya akipiga chapa ng'ombe katika uzinduzi wa zoezi la upigaji chapa ng'ombe wilayani Kiteto
HABARI KAMILI.......
Zoezi la upigaji chapa ng’ombe wilayani Kiteto lapokelewa vizuri baada ya Wafugaji kuelimishwa
Zoezi la upigaji chapa ng’ombe wilayani Kiteto limepokelewa vizuri na wafugaji baada ya wafugaji hao kuelimishwa juu ya umuhimu wa zoezi hilo.Akizungumza katika uzinduzi wa zoezi hilo lililofanyika tarehe 24/11/2017 katika kata ya Namelock Mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amesema kwamba zoezi hilo limepokelewa vizuri baada ya wafugaji kupewa elimu ya kutosha .
Kuhusu kusuasua kuanza kwa zoezi hilo mheshimiwa Magessa amesema kwamba, zoezi hilo limesuasua kwa sababu wahusika walitaka kulifanya bila kutoa elimu .Mheshimiwa Magessa anasema ‘‘kazi tuliyoifanya kwanza ni kuwapa wafugaji elimu ya kutosha.Tumewaita viongozi wa wafugaji,Maleigwanan na wafugaji ,tumekaa nao,tumezungumza nao, ,wakalifahamu zoezi hili lina faida gani na hasara gani , tukakubaliana. Kwa hiyo niseme tu kwamba faida za zoezi hili hazikuwa zimefahamika kwa wananchi vizuri, na hivyo ikaonekana kama wanalipinga.Kuna watu ambao walipita wakieleza kwamba ng’ombe akipigwa chapa atakaa miaka minne bila kuzaa , na wafugaji wakajua hii ni hasara. Kama ng’ombe atakaa miaka minne bila kuzaa ni hasara kubwa,lakini tulivyowapa elimu kwamba huu ni utambuzi wa mifugo kwa maana kwamba sasa tukishajua idadi ya mifugo ,tutawapa sehemu ya malisho, tutaandaa malisho, tutafika mahali kwenye masoko kwa hiyo wizi wa ng’ombe utapungua, na vitu vingine kama hivyo, wafugaji wakaona kwamba kumbe hili suala lilikuwa halikuelezwa vizuri, .Ndio sababu unaona sasa tunaanza kulifanyia ’’
Naye makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto mheshimiwa Hassan Benzi amesema kwamba wamekubaliana kuwa zoezi hilo la upigaji chapa liende sambamba na chanjo kwa ajili ya homa ya mapafu ambayo imekuwa tatizo kubwa sana kwa wafugaji wao. Kila mfugaji atachangia shilingi mia tano kwa ng’ombe mmoja kwa ajili ya kupata chanjo hiyo.
Katika hatua nyingine diwani wa kata ya Partimbo mheshimiwa Paulo Tunyoni ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya uchumi na mazingira amezungumza kuhusu watu waliokuwa wakieneza taarifa zisizofaa juu ya zoezi la upigaji chapa.Mheshimiwa tunyoni amesema ‘‘Wanasiasa waliokuwa wanasema kwamba chapa sio nzuri walikuwa hawajapata uelewa, lakini baada ya kuagiza kwenye baraza watu waelimishwe, tumeelewa kwamba chapa ina umuhimu mkubwa sana, umuhimu wa chapa ni nini, umuhimu wa chapa ni kujua idadi ya ng’ombe tulizonazo ambapo unatupeleka sisi kwenda sasa kuhangaika kuhakikisha kwamba mifugo yetu kutokana na wingi uliopo kwenye kijiji fulani inakuwa na maeneo ya kutosha kwa ajili ya malisho ’’ Mheshimiwa Tunyoni anaendelea kusema kwamba serikali imeliona hilo, na ndio maana imeagiza utekelezaji wa upigaji chapa ili kuhakikisha kwamba mifugo iliyo katika kijiji A inalingana na malisho yaliyopo katika kijiji A.
Kwa upande wake Afisa mifugo wa wilaya ya Kiteto ndugu William Msuya amesema kwamba anamshukuru Mungu zoezi hilo limeanza, lakini kulikuwa na changamoto kidogo kwa sababu ya uelewa wa vijana wa Kimasai wanaoitwa Nyangulo, ambao walitaka kuingilia zoezi bila ridhaa ya wazazi wao,lakini baada ya wazazi wao kuwapa elimu kama walivyopewa wao, zoezi limeenda vizuri. Kuhusu taarifa za upotoshaji wa zoezi hilo Msuya anasema ‘‘taarifa walizokuwa wanapata wafugaji kwamba mifugo ikipigwa chapa haizai ni upotoshaji na uzushi, ambao ulitengenezwa kwa lengo la kukwamisha zoezi hili .Lakini baada ya kupatiwa elimu na wataalamu na kupitia viongozi wetu wa kisiasa, mkuu wa wilaya, mwenyekiti wa halmashauri na viongozi wote kupitia baraza la madiwani, wamepata uelewa wa kutosha na zoezi limeenda vizuri’’.
Naye kiongozi wa mila ndugu Ngayoni Lebakari amesema kwamba zoezi hilo wamelipokea vizuri,baada ya viongozi wa mila kuitwa tarehe 18/11 /2017 kwenye ukumbi wa halmashauri ,ambapo walielezwa na kupewa elimu kuhusu zoezi hilo. Lakini kabla hawajapata elimu, wafugaji walikuwa wanasuasua kukubali ng’ombe wao kupigwa chapa. Walikuwa wakihoji kwamba chapa ikoje, kwanini hawajaelezwa,lakini baada ya kupata elimu kutoka kwa viongozi ambao walipewa elimu , walielewa kwamba upigaji chapa hauna madhara bali una faida, wamelipokea zoezi hilo vizuri.
Kuhusu ngombe walio nje ya wilaya, mkuu wa wilaya ya Kiteto mheshimiwa Tumaini Magessa amesema kwamba kuna ng’ombe ambao wako nje ya wilaya kwa ajili ya kutafuta malisho,lakini huu ni mwezi ambao wanaanza kurudi,kwa hiyo wameanza kupiga chapa wakijua kwamba ndani ya miezi miwili watakuwa wamemaliza zoezi kwa ng’ombe wote. Aidha mheshimiwa magessa amesema kwamba wako ng’ombe wanaozaliwa, na wako wanaoendelea kuja kutoka wilaya nyingine kwa sababu ya kununuliwa , na kwa hao pia watakuja kufanya zoezi hilohilo ,kama watakuja na chapa, maana yake makaratasi na hati ambazo watakuwa wamekuja nazo ndio zitawatambulisha kwamba wametoka wapi. Wilaya ya Kiteto ina ngombe zaidi ya 487,000, ambapo katika zoezi hilo ng’ombe 350,000 wanatarajiwa kupigwa chapa.
Kibaya-Kiteto
Anwani ya Posta: P.o.Box 98, Kibaya-Kiteto
Simu ya Mezani: +255 027-2552099
Simu ya kiganjani:
Barua Pepe: ded@kitetodc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halimashauri ya Kiteto.Haki zote zimehifadhiwa